Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli amesema serikali ya nchi hiyo haiwezi kutoa mikopo ya kimasomo
kwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu nchini humo.
Kiongozi huyo
alisema serikali yake imekuwa ikiongeza fedha za mikopo na kuwakopesha
wanafunzi wengi zaidi lakini akasisitiza kuwa sasa haitaweza kutoa
mikopo kwa wanafunzi wote wa vyuo vikuu.
"Nataka niwahakikishie
Serikali ya Awamu ya Tano inawapenda wanafunzi wa vyuo vikuu, lakini
lazima niwaambie ukweli Serikali haiwezi kutoa mikopo kwa wanafunzi
wote" alisema.
Dkt Magufuli alisema hayo alipokutana na wanafunzi
wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kilichopo katika
Manispaa ya Iringa ambapo alisikiliza kero zao mbalimbali zikiwemo
zinazohusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na mazingira ya kusomea,
kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu.
Rais Magufuli alisema utoaji wa mikopo ya elimu ya juu ni lazima ufuate taratibu pamoja na historia ya familia.
Alidokeza kwamba watakaopewa kipaumbele ni wale wanaosomea udaktari, ualimu na uhandisi.
"Hili suala la mikopo lina changamoto, ndiyo maana tunapotoa mikopo
tunaangalia historia ya mtu, ndiyo maana mtoto wangu hapati mkopo,"
alisema kwa mujibu wa gazeti la kibinafsi la Mwananchi.
"Huwezi
kumsomesha mtoto shule ya msingi ya binafsi, halafu baadaye aje aombe
mkopo. Hao waliokusomesha wapo wapi? Na kama hawapo tutataka
uambatanishe nyaraka kuonyesha hawapo."
Rais huyo alitania kwamba wanawe walijaribu kutumia ujanja wa kutumia jina la mama yao kupata mikopo lakini hawakufanikiwa.
"Hawa majamaa wajanja sana, tulijaribu kutumia jina la mama yao lakini bado wakawagundua," alisema.
Mwishoni
mwa mwaka jana, serikali ya Tanzania iliidhinisha Sh427 bilioni za
mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/18, lakini viongozi wa
wanafunzi walilalamika kuwa bajeti hiyo ilikuwa ndogo ukilinganisha na
mahitaji.
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya viongozi wa
wanafunzi walisema bajeti hiyo imekuwa ikizidi kupungua licha ya
wanafunzi kuongezeka.
Mkurugenzi wa haki za wanafunzi wa Mtandao
wa Wanafunzi Tanzania kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul
Nondo aliambia gazeti la Mwananchi wakati huo kwamba bajeti hiyo imekuwa
ikizidi kupungua licha ya wanafunzi kuongezeka.
Mwaka 2016/17 serikali ilitenga Sh483 bilioni kwa wanafunzi 120,000 za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
"Cha
kushangaza mwaka wa masomo 2017/18 wanafunzi wameongezeka na kufikia
122,000, lakini badala ya fedha za mkopo kuongezeka zimepungua na kuwa
Sh427 bilioni waombaji wakiwa 61,000 na Serikali imesema itawapa 30,000
pekee," alisema.
Lakini naibu waziri wa Elimu, William Ole Nasha
alisema Serikali imetenga fedha hizo kulingana na maombi ya Bodi ya
Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
Alisema: "Kuna vigezo ambavyo
vimewekwa na kulingana na vigezo hivyo bodi imejiridhisha fedha hizo
zinatosha, bodi ingeomba halafu Serikali ingepunguza lawama hizo
zingekuwa na tija.